Exodus 5

Matofali Bila Nyasi

1 aBaadaye Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’ ”

2 bFarao akasema, “Huyo Bwana ni nani, hata nimtii na kuruhusu Israeli uende? Simjui huyo Bwana wala sitawaruhusu Israeli waende.”

3 cNdipo Musa na Haruni wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Sasa turuhusu tuwe na safari ya siku tatu ya jangwani ili tukamtolee Bwana Mwenyezi Mungu wetu dhabihu, la sivyo aweza kutupiga sisi kwa tauni au kwa upanga.”

4 dLakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Musa na Haruni mnawachukua watu waache kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!” 5 eKisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.”

6 fSiku iyo hiyo Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu akawaambia: 7 g“Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali. Wao wakusanye nyasi zao wenyewe. 8 hLakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’ 9Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili kwamba wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.”

10Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa tena nyasi. 11Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’ ” 12Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi. 13Viongozi wa watumwa wakasisitiza, wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.” 14 iWasimamizi wa Kiisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?”

15Ndipo wasimamizi wa Kiisraeli wakaenda kumlilia Farao, wakisema: “Mbona umewatendea watumishi wako hivi? 16Watumishi wako hawapewi nyasi, hata hivyo tumeambiwa, ‘Tengenezeni matofali!’ Watumishi wako wanapigwa, lakini kosa ni la watu wako wenyewe.”

17Farao akasema, “Ninyi ni wavivu ndiyo sababu mnasema, ‘Turuhusu twende tukamtolee Bwana dhabihu.’ 18 jSasa nendeni kazini. Hamtapewa nyasi zozote, nanyi ni lazima mtengeneze matofali.”

19Wasimamizi wa Kiisraeli walitambua kuwa wako taabani walipoambiwa, “Hamtakiwi kupunguza idadi ya matofali mliotakiwa kutengeneza kila siku.” 20Walipoondoka kwa Farao, wakawakuta Musa na Haruni wakingojea kukutana nao, 21 kwakawaambia Musa na Haruni, “Bwana na awaangalie awahukumu ninyi! Mmetufanya tunuke kwa Farao na maafisa wake, nanyi mmeweka upanga mikononi mwao ili kutuua sisi.”

Mungu Anaahidi Ukombozi

22 lMusa akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Ee Bwana, mbona umewaletea watu hawa taabu? Kwa nini basi ukanituma mimi? 23 mTangu nilipomwendea Farao kuzungumza naye kwa jina lako, amewaletea taabu watu hawa, nawe kamwe hujawakomboa watu wako.”
Copyright information for SwhKC